Latest Post

 Washindi 20 wa kwanza katika kampeni ya ‘Miamala ni Fursa’ wazawadiwa

Bank of Africa -Tanzania imetoa zawadi kwa washindi wake 20 wa kwanza wa wiki kupitia kampeni ya huduma za kibenki kwa njia ya kidigitali iitwayo “MIAMALA NI FURSA”, ambapo kila mmoja amepokea zawadi ya Sh50,000 kwa kutumia huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi kupata huduma za huduma za kifedha.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya kampeni hiyo iliyozinduliwa Juni 4, 2025, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidigitali wa Bank of Africa-Tanzania, Bw Lameck Mushi, alisema kuwa mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni hiyo ya miezi mitatu, imepokelewa vyema na umma wa Watanzania.

Bw Mushi alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya jukwaa la benki kupitia simu kwa kuwazawadia wateja wanaofanya miamala ya kila siku. Juhudi hizi ni sehemu ya dhamira ya benki yao kuendeleza matumizi ya huduma za benki kidigitali na kuendeleza ujumuishwaji wa kifedha nchini Tanzania.

Afisa Mkuu wa Huduma za Kidigitali wa Bank of Africa-Tanzania, Bw Lameck Mushi, akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu kampeni ya “Miamala ni Fursa” kwa wateja wao kwa kutumia huduma za kibenki kwa kupitia simu zao za kiganjani , kushoto ni Afisa Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa RejaReja Asupya Nalingigwa na kulia ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano Nandi Mwiyombella.

“Tunafurahia mwitikio mkubwa tulioupokea hadi sasa. MIAMALA NI FURSA tayari imefanya huduma za kibenki kupitia simu kuwa za kuvutia na muhimu katika maisha ya kila siku ya wateja wetu,” alisema Bw Mushi.


Akiendelea, alisema ukweli kwamba “Wateja wanashinda zawadi za fedha kwa kufanya miamala ya kulipa bili au kutuma fedha unaonyesha kuwa vitendo vidogo, lakini vya mara kwa mara vina mchango mkubwa. Zaidi ya hapo, tumeongeza unafuu kwa wateja wetu kwa kupunguza ada za miamala ya Bank-to-Wallet kwa zaidi ya asilimia 50."


Kila wiki, wateja watano watakaokamilisha miamala mitatu ya Bank-to-Wallet (B2W) na muamala mmoja wa ziada (malipo ya bili, ununuzi wa muda wa maongezi au umeme) kupitia B-Mobile watakuwa na nafasi ya kushinda.

Mwisho wa kampeni hii, ambayo itaendelea hadi Septemba 2025, mshindi mkuu atajinyakulia zawadi ya pesa taslimu Sh5 milioni.

Afisa Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa RejaReja Asupya Nalingigwa, alisisitiza: “Lengo letu ni kufanya huduma za kibenki ziweze kufikiwa kwa urahisi, ziwe na manufaa na ziwaguse wateja wetu kwa ukaribu zaidi. Iwe uko mjini au kijijini, mradi una B-Mobile, unaweza kushiriki na kushinda.”

Ili kuhakikisha ushirikishwaji wa wote, Bank of Africa-Tanzania imehamasisha timu zake za matawi kote nchini kusaidia kuwaunganisha wateja wapya na kutoa mafunzo ya kutumia huduma hizo za kidigitali. Timu maalumu ya msaada wa kiufundi pia ipo tayari kusaidia kutatua changamoto zozote za upatikanaji na kuhakikisha uzoefu mzuri kwa watumiaji wote.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano Nandi Mwiyombella, aliongeza: “Kampeni hii si kuhusu zawadi pekee, bali ni kuhusu kuwapa nguvu wananchi. Kwa kuhamasisha matumizi ya huduma za kidigitali kwa njia shirikishi na rahisi, tunawasaidia Watanzania wengi zaidi kushiriki katika mfumo rasmi wa kifedha.”

Kwa zawadi zaidi za fedha na washindi wapya kutangazwa kila wiki, Bank of Africa -Tanzania inawaalika wateja wake wote kufanya miamala, kushinda, na kufurahia huduma za kibenki kwa urahisi kupitia simu zao.

 

 Kuhusu BOA Bank (T) Limited

BOA-Tanzania ni benki ya biashara binafsi inayotoa huduma kwa wateja wa kampuni kubwa, wateja wa kati (SME) na wateja wa rejareja nchini Tanzania. Ilianza shughuli zake Juni 2007 baada ya kununua Eurafrican Bank iliyokuwa ikifanya kazi nchini tangu Septemba 1995.

Benki hii ni sehemu ya kundi la Benki ya Afrika, ambalo lilianza shughuli zake mwaka 1982 nchini Mali.

Kundi hili linafanya kazi katika nchi 19 za Afrika, ikiwa ni pamoja na Afrika Magharibi, Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, pamoja na ofisi za uwakilishi Paris (Ufaransa), Hispania, London (Uingereza) na China. Tangu mwaka 2010, Benki ya Afrika imekuwa chini ya umiliki mkubwa wa BMCE Bank, benki ya tatu kwa ukubwa nchini Morocco, inayotoa huduma katika nchi 31 na mabara 4.

Kwa sasa, BOA-Tanzania ina matawi 17 ya rejareja, yakiwemo 8 Dar es Salaam na 9 katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Zanzibar na miji mingine mikubwa.


Mawasiliano ya Vyombo vya Habari:

Tovuti: www.boatanzania.com

Beatrice E. Mirigo – Maendeleo ya Bidhaa & Mawasiliano

Barua Pepe: beatrice.mirigo@boatanzania.co.tz

 

Simu: +255 699 000 260

 

 Mwisho………..

Na Mwandishi Wetu

Ikiwa imebaki miezi michache tu kufanya uchaguzi mkuu, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi na kuboresha huduma za kijamii nchini. Katika yote haya, imekuwa nyota inayong’aa si tu kwa Afrika Mashariki, bali pia kwa Bara la Afrika kwa jumla.

Utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii umefanyika kwa kuongozwa na sera, sheria, kanuni, taratibu na utekelezaji wa mikakati mbalimbali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo endelevu.

 Dkt Samia Suluhu Hassan alianzisha ajenda ya ‘4R’ kama nguzo muhimu ya maendeleo inayolenga maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya mustakabali wa kitaifa kisiasa. Lengo ni kuboresha mahusiano kitaifa, kikanda na kimataifa, na kuhakikisha tunajenga taswira mpya ya Tanzania, huku tukiendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi.

 Alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021, Dkt Samia Suluhu Hassan aliahidi kuimarisha demokrasia, haki za binadamu, kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ya maji, kuboresha usafiri wa umma na usafirishaji wa mizigo, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na mahusiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa, na kuendeleza mazuri ya awamu zilizopita, ikiwa ni pamoja na kuleta mambo mapya, yanayoendana na wakati tuliomo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madaktari na wauuguzi nchini.

Ukuaji wa Uchumi:

Serikali yoyote duniani katika ukusaji wa mapato ili kuimarisha uchumi wa ndani inategemea usimamiaji madhubuti wa sera, programu na mikakati mbalimbali kwa kuhakikisha mapato yanazidi kukua siku hadi siku. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21, serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi trilioni 20.59 na katika mwaka wa fedha 2023/24, ilikusanya kiasi cha Shilingi trillioni 28.83, ambazo ni mapato ya ndani. Pamoja na mambo mengine, katika ukusanyaji wa mapato, Shilingi trilioni 120.16 zilikusanywa kutoka vyanzo vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wizara, wakala wa serikali na serikali za mitaa.

 Elimu:

Katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu, serikali ya awamu ya sita iliamua kuondoa ada, na ilianza kusambaza vitabu, na kujenga madarasa, na pamoja na mambo mengine kufanya mapitio ya Sera ya Elimu, mafunzo ya ufundi na mitaala ili kuhakikisha wahitimu wanapata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipata maelezo jinsi miundombinu ya maji safi na salama inavyojengwa ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa Watanzania wote. Pamoja naye ni Waziri wa Maji Juma Aweso.

Katika sekta ya elimu, ambapo mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) yanalenga kuhakikisha wahitimu wanakuwa na maarifa, ujuzi, na maadili ili waweze kupenya katika soko la ajira.

Serikali iliamua kujenga shule 26 za wasichana za masomo ya sayansi kila mkoa, na shule 7 za wavulana kila kata nchi nzima, shule za msingi na sekondari 191,708 zilijengwa hadi mwaka 2020, na shule 254, 393 zimejengwa nchi nzima hadi mwaka 2025.

Pamoja na mambo mengine, shule za msingi mpya zilizojengwa mwaka 2025 ni 17, 986 na hadi mwaka 2020 zilizokuwepo shule 16,406. Idadi ya shule zote hizi ni matokeo chanya ya Ilani ya CCM.Vile vile serikali iliongeza vyuo vya ufundi stadi kutoka vyuo 662 mwaka 2020 hadi vyuo 860 mwaka 2024 kuendeleza ujuzi wa Watanzania katika sekta ya ufundi.

 Afya:

Msingi wa maendeleo ni pamoja na kuboresha afya ya umma. Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan iliwekeza katika sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya afya kutoka 8,783 mwaka 2020 hadi vituo vya afya 12, 846, na kuboresha miundombinu ya majengo, kununua vifaa tiba, kuboresha huduma za kibingwa na kusomesha madaktari na wahudumu wengine katika sekta ya afya.

“Miaka minne iliyopita idadi ya vifo vya akina mama wanaojifungua ilikuwa 556 kati ya 100,000, lakini kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, idadi ya vifo ilipungua hadi kufikia 104. Lengo la dunia ni vifo 70. Nina hakika tutafika huko na kuondoa kabisa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” alisema Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya mojawapo nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akimjulia hali mgonjwa katika moja ya hospitali za rufaa nchini. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye mfariji mkuu wa Watanzania


Maji:

Miaka michache iliyopita akina mama walikuwa wakiamka alfajiri na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo pia walikuwa hawana uhakika kama wangeweza kuyapata. Hadi kufikia mwaka huu, serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi ya usambazaji wa maji 2,331 katika miji na vijiji. Miongoni mwa miradi hiyo, ni ile ya Same, Mwanga na Korogwe ambapo wananchi wapatao 456,930 wamenufaika na miradi ya maji safi na salama.

Kilimo

Kwa miaka mingi kumekuwa na kauli mbiu mbalimbali za uhamasishaji wa kilimo tangu serikali ya awamu ya kwanza kama vile siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, na kilimo kwanza (ambayo ilikuwa kauli mbiu ya serikali ya awamu ya nne). Kilimo ni uti wa mgongo, na kauli mbiu hii inathibitisha utekelezaji wa sera ya kilimo kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza bajeti yake kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi Shilingi trilioni 1.24 mwaka 2024/25, na kuifanya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 26.2 kwa pato la taifa

Miaka ya nyuma Tanzania ilitofautisha mazao ya chakula, na ya biashara, lakini kwa sasa mazao karibu yote ni ya biashara, na mahitaji ni makubwa kwenye soko la nje, hata nyama kutoka Tanzania ambayo ni fursa muhimu kwa wakulima na wafugaji, lakini pamoja na mambo mengine, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17.1 mwaka 2021 hadi tani million 22.8 mwaka 2024, huku serikali ikitoa ruzuku ya Shilingi billioni 300 katika kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo huajiri takribani asilimia 65 ya nguvu kazi.

 Mifugo na Uvuvi

Serikali ya awamu ya sita imbadilisha mfumo wa kizamani na kuweka mfumo wa kisasa kuhakikisha ajira za Watanzania zinaendelea kuongezeka na usalama wa chakula una kuwa wa uhakika kwa kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo kutoka tani millioni 1.38 mwaka 2020 hadi tani millioni 2.6 mwaka 2025, na kuongeza maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta millioni 2.78 hadi hekta millioni 3.48. Ongezeko hili limepunguza migogoro ya wakulima na wafugaji, huku mauzo ya nyama nje ya nchi yakiongezeka pia kutoka tani 1,774 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 4.2 mwaka 2020 hadi tani 9,863.41 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 44 mwaka 2025.

 

Madini:

Sekta ya madini kwa muda mrefu ilionekana kama urithi wenye laana, lakini kwa sasa sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa imeboreshwa kupitia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2019, na mwaka 2022 mchango wake katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10.1 mwaka 2025. Masoko ya madini yameongezeka kutoka 41 mwaka 2021 hadi kufikia 43 mwaka 2025 na vituo vya madini vimeongezeka kutoka 61 hadi kufikia vituo 109. Uboreshaji katika sekta ya madini umesogeza huduma kwa wananchi, na kuongeza uwazi katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akizindua Mradi wa maji Butimba Mwanza.

Katika kuhakikisha mchango wa sekta hii unaendelea kukua kwa kasi, serikali ya awamu ya sita iliamua kununua mitambo 15 ya uchongoraji kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisambaza sehemu mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na kupanua uwazi wa sekta ya madini.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Amali-Mwamapalala katika kukamilisha ujenzi wa shule kama moja ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika sekta ya elimu nchini.

Pamoja na mambo mengine, baada ya kilio hicho cha muda mrefu na baadaye kwa kuwa na Sera ya Madini ya mwaka 2009 ya kuwawezesha Watanzania wazawa kushiriki katika sekta ya uchimbaji wa madini, kupata kazi za ukandarasi, zabuni na kutoa huduma mbalimbali kupitia Kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content) Watanzania wamekuwa wakipata ajira ndani ya migodi na nafasi za menejimenti kushikwa na wazawa.

 Kwa sasa serikali iko mbioni kujenga kituo cha kisasa cha maabara kwa ajili ya upimaji wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo ipo jijini Dodoma. Katika kipindi cha miaka minne ya awamu ya sita, chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan, serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kwa kutoa fursa kwa wazawa katika sekta ya madini kwa upatikanaji wa kazi migodini na marekebisho ya Uwajibikaji wa Jamii (CSR).

 Viwanda

Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kijani kupitia viwanda, na kupunguza tatizo la ajira nchini kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya viwanda 47,063 vilianzishwa. Kati ya hivyo, viwanda vikubwa ni 428, vya kati ni 1,393, vidogo ni 11,847 na vidogo sana ni 33,395, na pamoja na mambo mengine, kuendeleza kiwanda cha ngozi (Kilimanjaro Leather International Company Limited) kinachomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa asilimia 86, na Jeshi la Magereza kwa asilimia 14 kwa uwekezaji wa Shilingi billioni 152.96. Kwa hakika sekta ya viwanda ni injini kwa maendeleo ya taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akitizama ng’ombe kwenye moja ya programu za BBT za kunenepesha mifugo hapa nchini ili kukuza mahitaji ya mauzo ya nyama nje ya nchi na kuongeza kipato kwa wakulima na serikali kwa ujumla.

Makala haya hayawezi kutosha kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameisimamia kikamilifu ili kulinda na kuendeleza maliasili na utalii, uchukuzi, miundombinu, ardhi, nishati, mawasiliano na sekta zingine mtambuka kwa masilahi mapana ya nchini yetu.

Mwisho….


MJI WA SERIKALI, DODOMA –

Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa mafanikio yake katika kuimarisha mifumo ya tahadhari na ufuatiliaji wa majanga kupitia Kituo cha Dharura cha Taifa (Situation Room) kilichopo Mtumba, Dodoma.

Pongezi hizo zimetolewa na wataalamu kutoka Ghana, Togo na Burkina Faso waliopo nchini kwa mafunzo ya siku tatu ya kubadilishana uzoefu, yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maafa, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema kituo hicho kimeongeza uwezo wa taifa kutoa tahadhari mapema kwa wananchi na kuratibu mashirika mbalimbali kukabili majanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo hicho, Bi. Jane Kikunya, amesema wageni hao wameonesha nia ya kuiga mfumo huo katika nchi zao kutokana na mafanikio waliyojionea.

Aidha, wageni hao wameeleza kufurahishwa na jinsi taarifa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuwasilishwa kwa wananchi kwa haraka na kwa usahihi.










 NAMWANDISHI MAALUM

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. James Kilabuko amehimiza ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na majanga ya kibinadamu yanayochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa, kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuimarisha vituo vya ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema (Situation Room).

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya kubadilishana uzoefu, yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na UNDRR na Kituo cha Sayansi cha Afrika Magharibi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (WASCAL), Dkt. Kilabuko alisema mafunzo hayo ni sehemu ya kuimarisha uwezo wa kanda katika kukabili matukio ya majanga. Mafunzo hayo yalihusisha ujumbe kutoka Ghana, Togo na Burkina Faso.

Dkt. Kilabuko alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa majanga, kupitia vituo vyenye uwezo wa kukusanya taarifa mbalimbali, zikiwemo za hali ya hewa, maji, kijamii na kiuchumi, jambo linalosaidia kukabili majanga kama vile ukame na mafuriko.

 “Tunauzoefu mkubwa wa kiutendaji ambao unasaidia kuhakikisha vituo vyetu vinafanya kazi kwa ufanisi kwa kuratibu taasisi mbalimbali kukabiliana na majanga,” alisema Dkt. Kilabuko.






Serikali yazindua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini Nyamongo kwa udhamini wa Barrick

 Na Mwandishi Wetu, Nyamongo,

Serikali imezindua mafunzo ya siku 14 ya kuvijengea uwezo vikundi 48 vya vijana wachimbaji wadogo wa madini kutoka ukanda wa Nyamongo wilayani Tarime, mkoani Mara.

Mafunzo hayo yataanza kesho Juni 21, 2025, chini ya udhamini wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa kushirikiana na North Mara Trust Fund.

Vikundi hivyo vyenye wanachama 2,736 vilikabidhiwa leseni 96 za uchimbaji madini bure na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, mwanzoni mwa Mei 2025.

Hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo imefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe - Nyamongo leo, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (kulia), Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi na viongozi wengine wakifurahia uzinduzi wa mafunzo kwa wachimbaji wadago wa madini uliofanyika Nyamongo wilayani Tarime, Mara leo Juni 20, 2025.

Katika hotuba yake, Chikoka amewahimiza vijana hao kuhudhuria mafunzo hayo kikamilifu na kuyazingatia ili yawe muongozo na dira ya shughuli zao cha uchimbaji madini.Sambamba na hayo, amewataka kuepuka migogoro katika vikundi vyao na kutokubali kukatishwa tamaa katika hatua hiyo ambayo aliita safari ya mafanikio.“Kupitia kwenu tunatarajia kuona mabilionea wapya ndani ya Nyamongo. Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega, mkiwa na shida pigeni hodi mtafunguliwa na kusikilizwa,” Chikoka amewambia wachimbaji hao.Aidha, ameishukuru Barrick kwa kuridhia kutoa baadhi ya maeneo yake kwa ajili ya wachimbaji hao, akisema hatua hiyo itasaidia kukomesha tatizo la vijana kuvamia mgodi wa North Mara kwa kisingizio cha kukosa maeneo ya kuchimba madini.

 

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini waliohudhuria uzinduzi wa mafunzo yao.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kuboresha sekta ya madini nchini.Uhadi ambaye amemwakilisha Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, amesema wataendelea kuunga mkono jitihada hizo, na kwamba mafanikio katika mradi huo wa wachimbaji wadogo wa madini yanahitaji ushirikiano kati ya serikali na wadau.

 

Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Elisante Mshiu, amesema Serikali ya Tanzania inastahili pongezi kubwa kwa kuwa ya kwanza duniani kuanzisha hatua ya kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini.Dkt. Mshiu amesema mafunzo hayo yatahusu elimu ya uchimbaji na uchenjuaji madini, biashara, tabia ya fedha, afya na utunzaji wa mazingira, ushirikiano katika vikundi, sheria na miongozo mbalimbali ya uchimbaji madini.

 

Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wanaokwenda kunufaika na mafunzo hayo, wakiwemo Dominic Daniel, Bedi Elias, Careen John na Ester Max, wameeleza kupokea hatua hiyo kwa furaha, huku wakiomba hatua zilizobaki ziharakishwe ili waanze uchimbaji. “Tunaishukuru serikali kwa kutuletea mafunzo haya lakini tunaiomba isitucheleweshee hatua zinazofuata ikiwa ni pamoja na kutuonesha maeneo ya kuchimba na kusaidia vitendea kazi vya kisasa,” amesema Ester.

 

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini waliohudhuria uzinduzi wa mafunzo yao.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa makundi na siku tofauti kwenye kumbi za shule za sekondari Bwirege, Ingwe, Nyamongo, Nkenge, Kemambo na Julius Kambarage Nyerere zilizopo tarafa ya Ingwe.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo.

Picha ya pamoja ya viongozi walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo.


Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini (mbele) wakiwakilisha wenzao katika picha ya pamoja na viongozi.


 ...Ambapo Tsh 1.2 trilioni ilikwenda kwa makampuni ya wazawa

...Yawaasa watanzania kuchangamkia fursa migodini

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Kampuni ya Barrick Twiga imethibitisha kwa vitendo utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini kwa kufanya manunuzi Tsh 1.5 trillioni ambapo Tsh 1.2 trilioni 75% ilikwenda kwa makampuni ya watanzania wazawa kupitia kanuni ya maudhui ya ndani (Local Content).

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akifungua rasmi Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini.

Akitoa salamu kwa niaba ya wadhamini wa Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini nchini unaofanyika jijini Mwanza, Mkuu wa Kitengo cha Ugavi wa Barick North Mara, Enock Otieno alisema kwamba kwa ushirikiano wa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na wadau wengine wamefanikiwa kutekeleza kwa vitendo kanuni ya maudhui ya ndani (Local Content).

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akipata maelezo jinsi ya utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Ugavi, Barrick North Mara, Enock Otieno (mwenye miwani) kwenye Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta hiyo.

“Kwa kushirikiana na Wizara, Tume na wadau wengine tumefanya mikutano, warsha na makongamano kadhaa ili kuhamasisha na kukuza uelewa wa watanzania katika kushiriki kwenye shughuli za uchumi katika sekta ya madini ili kuchochea mabadiliko Chanya ndani ya nchini,” alisema Otieno

Aliongeza kwamba kampuni ya Barrick Twiga kwa kutambua madini ni maisha na utajiri wanatekeleza mradi wa barabara kutoka Kahama hadi kakola kilomita 73 kwa kutoa Tsh 83.36 billioni kwa minajili ya kuboresha miundombinu.

Mgodi wa Barrick North Mara umesisitiza kwamba ipo tayari kupokea na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini lakini muhimu ziwe na viwango vinavyohitajika,

Otieno alisema kwamba mgodi wa Barrick North Mara una fursa nyingi kwa ajili ya watanzania wazawa ili waweze kushiriki kwenye sekta ya madini.

“tupo tayari kupokea bidhaa zinazotokana na viwanda vya ndani ili umuhimu watanzania wajue mahitaji na ubora wa bidhaa kwa sababu usalama na afya za wafanyakazi ndani migodi ni kipaumbele cha kampuni ya Barrick katika migodi yake hapa nchini,” aliongeza

Otieno alisema kwamba tuna fursa nyingine ni uhitaji wa chuma kwenye mgodi wa Barrick North Mara na hii ni fursa kwa watanzania kuchangamkia kwa sababu pia kuna upatikanaji wa malighafi ya chuma kutoka Liganga.

Afisa Mawasiliano wa kampuni ya Barrick nchini, Neema Ndossi akipokea tuzo na cheti cha udhamini wa Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini nchini kwa niaba ya kampuni, unaofanyika jijini Mwanza.

Alifafanua kwamba ni muhimu watanzania kuzingatia weledi na kuunganisha nguvu zao ili kuweza kuanzisha viwanda vya chuma kwa sababu mahitaji ya malighafi hiyo migodini ni kubwa mno na fursa ya kipekee kwa watanzania wazawa kuanza kukua katika ukandarasi na huduma za migodini hapa nchini.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa watanzania wazawa kuanza kuingia kwenye sekta ya madini kwa sababu fursa zinapatikana mpaka kwenye ya uchongaji miamba kwenye mashimo ya chini bado kuna hitajika bidhaa na mitambo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji na cementi ,” alifafanua Otieno.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akipata maelezo jinsi ya utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Ugavi, Barrick North Mara, Enock Otieno (mwenye miwani) kwenye Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta hiyo.

Alisema kwamba umuhimu kwa watanzania wazawa kuzingatia ubora wa bidhaa na uendelevu wa usambazaji wa huduma husika ili kuweza kujenga uaminifu na uwezo kwa wakandarasi wa ndani kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Naye , Meneja Mahusiano ya Jamii,wa Barrick North Mara, Franscis Uhadi kupitia alisema kwamba kampuni hiyo ya Barrick ambayo inamiliki migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ambao huo katika hatua za mwisho za ufugaji inaendelea kutekeleza kanuni zote za Maudhui ya Ndani (Local Content) na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

“Kampuni ya Barrick inatekeleza kwa vitendo ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini kwa kufanya kazi na makampuni ya wazawa na kuendelea kuwajengea,”

“Jumla ya makampuni ya ndani 706 imefanya kazi na migodi ya barrick na kuna makampuni 603 ni kampuni za wazawa na bado tutaendelea kufanya kazi na makampuni ya kitanzania kama sehemu ya kuwajengea uwezo,” aliongeza

Kwa upande wake, Mgeni rasmi wa Jukwaa hilo la nne la ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini, Waziri wa Madini, ,  Anthony Mavunde  alisema kwamba sekta ya madini imeweza kuchangia 9.0 % ya pato la taifa mwaka jana.

“mafanikio katika sekta ya madini ni makubwa na mpaka sasa ninavyozungumza sekta hii ya madini imechangia Tsh 985 billioni kwenye mfuko mkuu wa serikali haya ni mafanikio makubwa sana kwenye sekta ya madini,” alisema Mavunde.

Aliongeza kwamba serikali ya awamu ya sita chini Dkt Samia Suluhu Hassan ilitoa maelekezo ya kuweka akiba ya dhahabu na ndani ya miezi nane Benki kuu ya Taifa (BOT) ina akiba ya dhahabu ya Tani 5.2.

“Sekta hii ya madini inakua kwa kasi kubwa pamoja na mambo mengine kuna viwanda tisa vinajengwa vya kuchakata na kusafisha dhahabu ili kukuza mnyororo wa dhamani,” aliongeza Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde alisema kwamba katika utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini kupitia kanuni ya maudhui ya ndani (Local content) ambapo kuna watanzania 16,874 ambao wameajiriwa kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Alifafanua zaidi kwamba ni muhimu watanzania ambao ni watoa huduma wazingatie weledi kwenye kazi ya utaoji huduma migodini (compliance) na kujenga utamaduni wa kushirikiana kwa kushikana mikono ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.

“ndugu zangu watanzania changamkieni hizi fursa kwenye sekta ya madini kwa kushirikiana na serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wazawa kuweza kufanya kazi kwenye migodi na kuwajengewa uwezo pamoja na kuhakikisha kwamba taasisi za fedha zinawakopesha,” alisisitiza

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo alisema kwamba sekta ya madini imeendelea kuchangia mapato ya serikali, kutoa fursa za ajira kwa watanzania kupitia maudhui ya ndani (Local content), kukuza ujuzi kwa wazawa na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.

“Malengo ya sera ya madini 2009 pamoja mambo mengine ila muhimu wa kuifunganisha na sekta zingine za kiuchumi ili kuchochea ukuaji wa sekta zingine na kuchangia maendeleo ya taifa, alisema Mbibo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Madini na Biashara kutoka Tume ya Madini, CPA, Dkt Venance Kasiki, alisema kwamba watanzania wanayo fursa ya kwenda kwenye mgodi wa Buzwagi ambao upo kwenye hatua za mwisho za ufugaji.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa watanzania wazawa kwenda kwenye eneo la Buzwagi ambapo kuna miundombinu bora na ya kisasa kama vile maji, umeme na Barabara kwa ajili ya kufanya uwekezaji,” alisema Dkt CPA Kasiki

Alisema kwamba eneo la mgodi wa Buzwagi watanzania wanaweza kuanzisha viwanda vya bidhaa kwa ajili ya kuhudumia migodi kadhaa ya hapa nchini na kutokana na eneo la Buzwagi ambalo lina Hecta

Alisema kwamba pamoja na mambo mengine eneo la Buzwagi lenye hecta 3365 ambalo ni maalum kama Kongani ya uwekezaji na viwanda (BSEZ) ina fursa ya zaidi ya kujengwa sio tu viwanda vya bidhaa kwa ajili ya migodini hata viwanda vya vipuri kwa ajili ya mitambo ya migodini.

Alisema kwamba hii ni fursa ya kipekee kwa watanzania kuendelea kuunganisha nguvu zao kutokana na miundombinu mizuri na bora kwenye eneo la Buzwagi ni kuharakisha uanzishwaji wa viwanda na kutoa na kutoa bidhaa zenye ubora na viwango.

Dkt CPA Kasiki alisema kwamba Tume hiyo imeendelea kutoa mafunzo na elimu kwenye makampuni, taasisi za elimu mbalimbali na jamii kwa ujumla ili uelewa wa Maudhui ya Ndani (Local Content) ili watanzania wapate uelewa zaidi kuhusu kanuni hiyo.

“Serikali kupitia Tume ya Madini imejikita na ina wataalamu wa kutosha wa kutoa elimu kuhusu Maudhui ya Ndani (Local Content) ili watanzania waweze kupata uelewa na kuingia kwenye sekta ya madini kwa ajili ya kupata kazi za kutoa huduma, ajira na ukandarasi wa shughuli mbalimbali kwenye migodi ambayo ipo hapa nchini,” aliongeza Dkt CPA Kasiki

Aliongea kwamba ni umuhimu kwenye hii ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini moja ya nyenzo muhimu ni ya kuungana (Joint venture) kwa maana ya kutunisha mtaji ili kuweza kupata kazi kwenye migodi iliyopo hapa nchini.

Dkt CPA Kasiki alifafanua kwamba serikali iliamua kuja na kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content) baada ya kilio cha umma (Public Outcry) kuhusu kwa watanzania hususani jamii inayozunguka migodi kutokunufaika na uwepo wa rasilimali madini.

“Baada ya kilio hicho cha muda mrefu na baadaye kuja kwa sera ya madini ya mwaka 2009 ya kuwawezesha watanzania wazawa kushiriki katika uchimbaji wa madini, kupata kazi za ukandarasi, zabuni na kutoa huduma mbalimbali,” alisema Dkt Kasiki

Dkt CPA Kasiki aliongeza kwamba pamoja na mambo mengine sheria ya madini 2019 na 2022 ili kuja ili kutatua matatizo na kero za ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini ili kupanua wigo na utatuzi wa changamoto hizo.

Aliongeza kwamba fursa za kukuza mnyororo wa thamani kwa watanzania kupitia sekta ya madini ni kubwa na pamoja mambo mengine fursa za kazi kama vile, mitambo ya migodini, Tehama, ujenzi wa viwanda vya kutoa bidhaa kwenye migodi, usafi na ufuaji wa nguo, famasi na tiba na huduma ya chakula. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt Janet Lekashigo alitoa wito kwa wadau kuendelea kushiriki kwenye Jukwaa la madini ili kuleta na kuchochea fikra za nafasi ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini nchini.

Dkt Lekashigo alisema kwamba jukwaa hilo ni kuchochea fikra mpya na majadiliano ya kitaaluma ili kuweza kusaidia watanzania kushiriki kwenye uchumi wa sekta ya madini.

“Jukwaa hili la nne ni la majadiliano, mawazo na kuleta fikra Chanya ili kuchochea mabadiliko ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini ili waweze kunufaika na rasilimali za madini hayo kwenye maeneo yao,” alisema Dkt Lekashigo

Aliongeza kwamba umuhimu wa Jukwaa hilo ni kuja pia na mapendekezo mbalimbali ya namna bora ya kuwawezesha na kufungua milango ya watanzania wazawa kufanya kazi zaidi za ukandarasi na zabuni kwenye migodi hapa nchini.

Dkt Legashiko alisema kwamba Tume hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wote kwenye sekta ya madini hususani sekta binafsi kupitia Maudhui ya Ndani (Local content) kuhakikisha dira ya madini ni maisha ni utajiri inakamilishwa kikamilifu kwa kuwashirikisha watanzania wazawa kwenye sekta ya madini nchini.

Mwisho

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.